ARGENTINA FAINALI NA MESSI AVUNJA REKODI NA KUWA MFUNGAJI WA MUDA WOTE.
Asubuhi hii, Nusu Fainali ya Kwanza ya COPA AMERICA CENTENARIO inayochezwa huko Marekani imechezwa katika uwanja NRG Stadium, Houston mbele ya Mashabiki 70,858 na Wenyeji USA kupokea kichapo cha paka mwizi cha mabao 4-0 na Argentina.
Hii itakuwa ni Fainali ya Pili mfululizo kwa Argentina ambao Mwaka Jana walitinga kufungwa na Chile.
Ezequiel Lavezzi aliipa Argentina Bao la Kwanza Dakika ya 3 tu na Lionel Messi kufunga jingine Dakika ya 32, Bao ambalo limemfanya awe ndie Mfungaji Bora katika Historia ya Argentina akiwa na Mabao 55 akimpiku aliekuwa na Rekodi hiyo Gabriel Batistuta aliefunga Bao 54.
Bao hilo lilifungwa kwa Frikiki murua.
Hadi Mapumziko USA 0 Argentina 2.
Dakika ya 50, Gonzalo Higuain akaipa Argentina Bao la Tatu na kufunga tena Bao la 4 Dakika ya 86.
Nusu Fainali nyingine itachezwa Usiku wa Leo huko Soldier Field, Chicago kati ya Colombia na Mabingwa Watetezi wa Copa America, Chile.


VIKOSI VILIVYOANZA:
United States: Guzan; Yedlin, Cameron, Brooks, Johnson; Zusi, Beckerman, Bradley, Zardes; Dempsey, Wondolowski
Akiba: Besler, Birnbaum, Nagbe, Howard, Orozco, Kitchen, Pulisic, Castillo, Horvath

Argentina: Romero; Mercado, Otamendi, Funes Mori, Rojo; Augusto, Mascherano, Banega; Messi, Higuain, Lavezzi
Akiba: Roncaglia, Cuesta, Lamela, Kranevitter, Aguero, Biglia, Maidana, Guzman, Pastore, Andujar, Di Maria

Mashindano haya Copa América Centenario ni mahsusi kusheherekea Miaka 100 ya Copa America, Mashindano ya Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani ya Kusini, CONMEBOL, ambayo yalianzishwa Mwaka 1916.
Hii ni mara ya kwanza kwa michuano hii kuchezwa nje ya Marekani ya Kusini.
Haya yatakuwa ni Mashindano ya 45 kufanyika na kawaida yake hufanyika kila baada ya Miaka Minne lakini safari hii CONMEBOL na CONCACAF, Shirikisho la Soka la Nchi za Marekani ya Kaskazini, Kati na Nchi za Visiwa vya Caribbean, walikubaliana kuandaa Mashindano maalum.
Safari hii michuano hii itakuwa na Nchi 16, badala ya 12 za kawaida, kwa kushirikisha Nchi 10 kutoka CONMEBOL na 6 za CONCACAF.
Kawaida Mshindi wa Copa America huiwakilisha Marekani ya Kusini kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Shirikisho lakini Mshindi wa Copa América Centenario hatapewa hilo kwani Mwaka Jana Chile, wakiwa Nyumbani kwao, ndio walitwaa Copa America ya kawaida na wao ndio watashiriki Mashindano ya FIFA ya Kombe la Shirikisho Mwakani, 2017, huko Russia.
Post a Comment
Powered by Blogger.