Kenya: Baa Inayoongeza Mkojo Kwenye Pombe Yapokonywa Leseni


KAMATI ya kiusalama katika Kaunti ya Murang’a ikiongozwa na Kamishna Kula Hache Jumamosi imetangaza kufutiliwa mbali kwa leseni ya baa ambayo mhudumu wake alinaswa akiwauzia walevi pombe iliyochanganywa na mkojo.

Bi Hache akitoa taarifa hiyo afisini mwake mjini Murang’a alisema kuwa mhudumu huyo alifikishwa mahakamani Aprili na ambapo alipigwa faini ya Sh40,000.

“Lakini kwa upande wetu kama kamati tumeafikiana kwa kauli moja baa hiyo ipigwe marufuku na kwa sasa ilani hiyo imepelekwa hadi katika kituo cha polisi cha Maragua na kwa sasa nimethibitisha baa hiyo imefungwa,” akasema.

Alisema kuwa kamati hiyo pia imeorodhesha mjengo ambao ulikuwa ukihifadhi baa hiyo inayojulikana kama Mahewa kuwa haufai kuwekwa
biashara ya kuuza pombe.

“Sio tu kupiga mrufuku baa hiyo. Hata mwenye nyumba hiyo hanaruhusa ya kukodisha jumba hilo kuwekwa biashara ya baa,” akasema.

Alisema hatua kama hiyo itazima wafanyabiashara matapeli kuingia katika biashara ya uuzaji vileo na hatimaye kuandamwa na tama ya faida
kiasi kwamba “wanaweza wakatumia hila hata zisizo na ubinadamu kuafikia faida hizo.”

Mhudumu huyo wa kike aliyetambuliwa kama Bi Esther Njeri alinaswa Aprili akiuza pombe wakati wa asubuhi kinyume cha sheria na
ambapo mmoja wa wateja wake aliteta kuwa pombe yake aina ya Senator Keg aliyokuwa ameuziwa ilikuwa ikinuka mkojo.

Akithibitisha kisa hicho wakati huo, kamanda wa polisi katika Kaunti hiyo Bi Naomi Ichami alisema shida ilitokea wakati mteja huyo alikataa
katakata kulipia kikombe cha pombe hiyo alichokuwa ameagiza huku mhudumu akimkabili amlipe.

“Wateja wengine waliingilia kati na wakasisitiza kuwa ni lazima wangefanya msako ndani ya kaunta ya baa hiyo ili wapate ukweli wa
mambo kama kwa uhakika walikuwa wakiuziwa mkojo,” akasema.

Bi Ichami alisema kuwa hali ya mshikemshike ilizuka ndani ya baa hiyo na mhudumu huyo wa kike akapigia maafisa wa polisi simu akidai kuwa alikuwa amevamiwa na genge la wizi ndani ya baa hiyo.

“Mhudumu huyo alipiga simu akilalamika kuwa alikuwa amejitokeza ndani ya baa hiyo kutekeleza usafi huku akifanya hesabu zake za mauzo ya usiku wa kuamkia jana alipovamiwa na genge hilo,” akasema.

Sh30 kwa kila kikombe
Hata hivyo, maafisa waliowasili walichanganyikiwa kwanza walipokuta wateja hao ambao walikuwa sita wakiwa na vikombe vidogo vya pombe vinavyouzwa kwa Sh30 kwa kila kimoja.

“Maafisa hao waligundua kuwa kulikuwa na biashara iliyokuwa ikiendelezwa kinyume cha sheria ndani ya baa hiyo na ndipo wakawahoji
vijana hao ambao walikuwa wamemthibiti mhudumu huyo,” akasema.

Baada ya kusikiliza kwa makini taarifa za tetesi kutoka kwa vijana hao, maafisa hao waliingia katika kaunta ya baa hiyo na ndipo
walikumbana na kibuyu kilichokuwa na mkojo!

“Ung’amuzi wetu kufikia sasa ni kuwa mkojo huchanganyika na pombe hiyo ya Senator Keg kwa kuwa yako na rangi sawa. Huu ni utundu wa hali ya juu wa kusaka faida na kwa uhakika hatujachukulia suala hilo kwa urahisi,” akasema. 


  Powered By Red Gold.
 Je, Unajua Kuwa @RedGoldtz Wanatoa Mtonyo Kwa Ajili Yako?
Nunua Red Gold Tomato Au Chill Ujishindie Mamilioni Leo..!!
‪#‎LadhaNaMtonyo‬
Bonyeza Hapa Kujua Zaidi
Post a Comment
Powered by Blogger.