Ivi Ndivyo Wapinzani Wa Yanga Kombe La Shirikisho Afrika Kujulikana Leo.


WAPINZANI wa Yanga katika hatua ya makundi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanatarajiwa kujulikana leo. CAF inatarajiwa kupanga makundi ya michuano hiyo na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika makao makuu ya CAF, Cairo nchini Misri saa 6:30 mchana.

Yanga ni miongoni mwa timu nane zilizotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuifungisha virago timu ya Angola ya Sagrada Esperanca kwa kuifunga jumla ya mabao 2-1.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 kabla ya kufungwa 1-0 na kusonga mbele. Yanga ilitinga hatua ya makundi baada ya kutolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-2 na Al Alhly ya Misri.


Yanga ilitoka sare ya 1-1 nyumbani kabla ya kufungwa 2-1 Misri. Mbali ya Yanga, timu nyingine zilizofuzu kwa hatua hiyo hivyo kuweza kupanga na mabingwa hao wa Tanzania ni pamoja na mabingwa watetezi, Etoile du Saleh ya Tunisia na Medeama ya Ghana.

Nyingine ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyoangukia katika michuano hiyo baada ya kuvuliwa ubingwa wa Afrika na Wydad de Casablanca ya Morocco hivi karibuni.

Pia zimo Al Ahly Tripoli ya Libya, MO Bejaia ya Algeria na mbili kutoka Morocco, Kawkab Marrakech na Fus Rabat.
 Kwa kufuzu kucheza hatua hiyo, Yanga imejihakikishia kitita cha dola 150,000 (Sh milioni 315) na kila hatua itakayopiga katika michuano hiyo ambayo bingwa wake atazoa dola 625,000 (Sh bilioni 1.3), itazidi kuogelea utajiri wa fedha.
 Mshindi wa pili atapata dola 432,000 (Sh milioni 907) wakati timu zitakazoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kila kundi zitapata dola 239,000 (Sh milioni 500).
Post a Comment
Powered by Blogger.