CECAFA YA MUSONYE NA HADITHI ZA KABURI LA SOKA.

CECAFA YA MUSONYE NA HADITHI ZA KABURI LA SOKA.

Mwaka 1927 ilianza moja ya michuano mikongwe barani Afrika kama siyo duniani kwa ujumla ikijulikana kama Gossage cup ikishindanisha mataifa ya Afrika mashariki, mpambano wa kwanza ukiwa kati ya Kenya na Uganda.
Michuano hii iliasisiwa na kudhaminiwa na kampuni ya utengenezaji sabuni iliyokuwa ikimilikiwa na raia wa Uingereza ambapo mmoja wa wamiliki aliitwa William Gossage na jina lake ndilo lililoitwa michuano hiyo kwa heshima yake.
Miaka takribani hamsini hivi baadae ndipo michuano hii ilizaa wazo la kuanzisha baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati maarufu kama CECAFA.
Kufikia mwaka huu baraza hili lina wanachama wapatao kumi na wawili. Linaratibu na kuendesha michuano ya vilabu iitwayo Kagame cup na ile ya timu za taifa iitwayo "CECAFA senior challenge cup".
Hata hivyo ukanda huu wa soka uko chini sana katika maendeleo ya mpira wa miguu Afrika na duniani kwa ujumla. Hivi sasa Uganda ndiyo inayoonekana kuwa juu ktk msimamo wa viwango vya ubora wa soka duniani kwa kushika nafasi ya sabini na mbili (72) kwa takwimu zilizotolewa mwezi Mei.
Kwa upande wa vilabu ukiacha vilabu vya Sudan kaskazini nchi nyingine zote hazina zinakofika.

 Ni Gormahia ya Kenya na Simba ya Tanzania angalau ndivyo vilabu kutoka ukanda huu ambavyo vimewahi kuweka historia ya kucheza fainali ya michuano ya vilabu miaka mingi iliyopita ambayo hata sasa imefanyiwa marekebisho makubwa.
Swali langu kubwa ni kwamba CECAFA inafanya nini au inasaidiaje kuinua soka ktk ukanda huu?
Michuano ya vilabu "Kagame cup" imekuwa ni michuano ya kuwapatia kipato baadhi ya watu. Imefikia mahali yanatengezwa mazingira kwa mwenyeji kucheza fainali ili mradi zipatikane fedha za kutosha kutajirisha watu wachache. CECAFA inauza majina wasiyoyatengeneza wala kuyatolea jasho.

 Inasubiri Simba na Yanga zisajili ili wao waje wafaidike na usajili huo pamoja na kunyonya jasho la wapenda soka Tanzania.
Nicholaus Musonye amegeuka kuwa mungu mtu ktk shirikisho hilo kwakuwa kila analolisema na kulipanga ndilo linalofanyiwa kazi bila kujali yana faida au hasara kwa soka letu.
CECAFA haina ratiba inayoeleweka wala mpango wowote.
Hadi wakati huu haijulikani michuano ya "Kagame cup" itafanyika wapi na lini, tayari kulikuwa na tetesi kwamba huenda michuano hiyo ikafanyika Tanzania, lakini kitega uchumi kikubwa cha Musonye, klabu ya Yanga tayari imefuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho barani Afrika hivyo nadhani Yanga haiwezi kushiriki "Kagame cup" hivyo kuathiri mapato ya Musonye endapo michuano hiyo itafanyika Tanzania.
Ukilinganisha wakati wa "Gossage" na sasa hivi wakati tukiwa na CECAFA tofauti ni majina na uwingi wa washiriki lkn lengo ni lile lile.
Hakuna udhamini kwa mashindano yetu, wala hakuna hakuna ushauri wa kitaalamu toka CECAFA, wala shirikisho lenyewe halina nguvu za kisheria ktk mfumo wa FIFA hivyo hata mashindano yake hayana faida kwakuwa hayatambuliki.
Kwa ujumla CECAFA ya Musonye inahitaji marekebisho ya kimfumo, kiutendaji na kimkakati, kama sivyo badala ya kuwa msaada litakuwa kaburi la soka letu.


Imani K Mbaga.
 0717469593
Post a Comment
Powered by Blogger.