Haya Ndo Maamzi Ya Rais Omar Al-Bashir Kuachia Madaraka 2020 Sudan.

Rais wa Sudan Omar Al-Bashir.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir ameambia BBC kwamba ataondoka madarakani mwaka 2020 muhula wake wa sasa utakapomalizika.
Bw Bashir pia amekanusha tuhuma kwamba wanajeshi wake wamekuwa wakitekeleza dhuluma kwenye vita vipya dhidi ya wanavijiji weusi katika eneo la Darfuf, magharibi mwa nchi hiyo.
Kiongozi huyo anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita.
Bw Bashir amekuwa madarakani tangu 1989. Alishinda uchaguzi mkuu Aprili mwaka jana.
Ameambia mwandishi wa BBC Thomas Fessy kwamba kazi yake “inachosha” na kwamba muhula wake wa sasa utakuwa wa mwisho.
“Mwaka 2020, kutakuwa na rais mpya na nitakuwa rais wa zamani,” amesema.
Hata hivyo, wakosoaji wake watasema tayari amewahi kuahidi kung’atuka awali lakini baadaye akakosa kutimiza ahadi hiyo, mwandishi wa BBC anasema.
Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 2.5 milioni wamefurushwa makwao Darfur tangu 2003, zaidi ya 100,000 wakitoroka makwao mwaka huu pekee.
Rais Bashir amesema hakuna haja ya kuwa na walinda Amani wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kutoa misaada eneo la Darfur.
Amekana taarifa za kutekelezwa kwa dhuluma zaidi maeneo ya milima ya Jebel Marra ambapo wanajeshi wa serikali walianzisha operesheni Januari.
Bashir anatafutwa na Mahakama ya ICC.

"Madai haya yote hayana msingi, ripoti hizo zote hazina ukweli,” amesema.
"Namtaka yeyote azuru vijiji vilivyotekwa na wanajeshi, na wanioneshe kijiji kimoja ambacho kimeteketezwa.
"Kusema kweli, hakujakuwa na mashambulio yoyote ya kutoka angani.”
Rais huyo amesema wote waliotoroka mapigano walikimbilia maeneo yanayodhibitiwa na serikali na kwamba hiyo ni ishara tosha kwamba serikali haiwashambulii raia.
Rais Bashir pia amesema makadirio ya UN kwamba zaidi ya watu 100,000 wametoroka makwao eneo la Darfur tangu Januari kwa sababu ya mapigano “yametiwa chumvi na si ya kweli”.
Ni watu wachache sana ambao wametoroka makwao na wamekimbilia maeneo yanayodhibitiwa na wanajeshi wa serikali au maeneo ambayo yana wanajeshi wa kulinda amani wa UN, kikosi ambacho hujulikana kama Unamid.
Amesema wanajeshi wa UN na walinda amani wa umoja huo hawana jukumu kubwa la kutekeleza na wanafaa kuondoka nchini humo.
Rais Bashir.
Aidha, amesema mashirika ya kutoa misaada yanayotoa misaada kwa wakazi eneo la Darfur hawana jukumu la kutekeleza kwa sababu hakuna uhaba wa chakula Darfur.
Bw Bashir amesema makadirio ya Umoja wa Mataifa kwamba watu 2.5 milioni wanaishi kambini eneo la Darfur si ya kweli na kwamba idadi ya kweli ni watu karibu 160,000.
Bw Bashir alipata asilimia 94 ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka jana ambao ulisusiwa na upinzani.


 Source bbc.
  Published By: Alex Sonna.
 UnawezaKuzipata Story Zote Za Ndani Na Nje Ya Bongo Kwa Kujiunga
 Na SeetheAfricanLinkKwenye:
Facebook|Twitter|Instagram|YouTube|Audiomack
Powered by Blogger.