Hatari Kipindupindu Chaua Watu 45 Visiwani Zanzibar.

Watu zaidi ya 45 wamefariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu visiwani Zanzibar katika kipindi cha miezi miwili, shirika la habari la AP limeripoti.
Shirika hilo la habari limemnukuu afisa wa afya visiwani humo anayesema vifo hivyo vimetokea mwezi Machi na Aprili.
Muhammed Dahoma, ambaye ni mkurugenzi wa anayeangazia kuzuia maradhi katika wizara ya afya, anasema watu karibu 3,000 wamelazwa hospitalini baada ya kuugua.
Ameongeza kuwa serikali ya Zanzibar imechukua hatua kukabiliana na mlipuko huo.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kupiga marufuku uuzaji wa chakula na juisi maeneo ya wazi.
Taarifa kutoka visiwani humo zinasema serikali pia imeamuru kufungwa kwa shule zote kwa muda usiojulikana.
Waziri wa elimu Riziki Pembe Juma, amenukuliwa na shirika la habari la Uchina la Xinhua, akisema uamuzi huo umetolewa baada ya kubainika kwamba wanafunzi ni miongoni mwa watu walioathiriwa zaidi na ugonjwa huo.
“Tumejaribu kudhibiti hali, lakini kwa maslahi ya watoto wetu, watakuwa salama zaidi wakisalia nyumbani,” amesema kupitia taarifa, kwa mujibu wa Xinhua.
Ameongeza kuwa baadhi ya shule zimeathirika zaidi kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Kisiwa cha Unguja ndicho kilichoathirika zaidi ambapo watu 20 wamefariki na 400 kuambukiwa tangu Januari mwaka huu.
Waziri wa afya Mahmoud Thabit Kombo aliambia gazeti la serikali la Daily News wiki jana kwamba ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni visiwa vidogo na watu si wengi sana “kipindupindu sasa ni tishio kubwa”.
Mlipuko wa kipindupindu ulianza mwaka jana.
Kufikia Oktoba, visa 140 vya maambukizi vilikuwa vimeripotiwa katika visiwa hivyo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Powered by Blogger.